Idhaa ya kiswahili ya BBC imezindua rasmi studio zake za jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo ni matokeo ya mkakati na uwekezaji wa miaka
mingi wa
shirika la BBC duniani kuhakikisha kuwa matangazo yake yanawafikia
wasikilizaji katika hali ya ubora wa hali ya juu na ya kisasa zaidi.
Katika hafla hiyo iliyoandaliwa katika ofisi hizo hizo mpya zilizoko
eneo la Mikocheni, mkuu wa kitengo cha uandishi wa habari katika BBC,
Nicki Clarke, ameshukuru serikali ya Tanzania, kwa kuwaruhusu kujenga
studio hizo za kisasa zitakazoinua tasnia ya habari nchini humo na uhuru
wa habari kwa ujumla.
Naye mkuu wa ofisi ya Dar es Salaam, Hassan Mhelela mbali na kuwataka
wafanyakazi wa BBC Tanzania, kuzidi kuonyesha ushirikiano pamoja na
utendaji kazi wa pamoja, pia ametangaza kuanishwa rasmi kwa ushirikiano
kati ya BBC na chuo kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha uandishi wa
habari.
Ushirikiano huo amesema kuwa unalenga kusaidia kutoa mafunzo kwa
wandishi wa habari chipukizi walioko mafunzoni katika chuo hicho, ambao
kwa nyakati tofauti, watakuwa wakijiunga na BBC ili kupata mafunzo
katika uandaaji vipindi vya redio na televisheni pamoja na utangazaji.
Kwa upande wa BBC, kuanzishwa kwa ofisi hii, yenye studio za kisasa
kabisa za redio na televisheni mbali na kuongeza ubora wa vipindi lakini
pia kutawezesha matangazo ya redio na televisheni kufanyika moja kwa
moja kutokea Dar es Salaam.
Na kuanzia sasa matangazo ya Amka na BBC yatakuwa yakiandaliwa Dar es Salaam.
Itakumbukwa kuwa Tanzania mbali na kuwa na wasikilizaji wengi wa
idhaa ya kiswahili ya BBC, lakini pia ndiko kunakozungumzwa zaidi lugha
ya kiswahili.
Tanzania pia ina rekodi ambapo mtangazaji wa kwanza au sauti ya
kwanza iliyosikika mwaka 1957, ilikuwa ya mtanzania Oscar Kambona ambapo
alikuwa mwanafunzi mjini London.
Chanzo: BBC Swahili
No comments:
Post a Comment