Katika hali isiyo ya kawaida, Limu Jumanne mkazi wa mkoani Singida, amemtimua na kumrejesha mkewe kwa wazazi wake akidai ni
mvivu na mzembe kutokana na kushindwa kudhibiti kundi la fisi walioshambulia na kuua ndama sita wa ng’ombe akiwa machungani.
Limu anayeishi kitongoji cha Itigi, kijiji cha Irisya wilayani Singida anadaiwa kufanya ukatili huo mwishoni mwa wiki baada ya mkewe kurejea nyumbani jioni akitokea machungani huku ndama sita wakiwa wamepungua.
Aliyekutwa na mkasa huo alitajwa kuwa ni Hamida Sinde, ambaye inadaiwa kuwa siku ya tukio majira ya saa 12 jioni akiwa anachunga ng’ombe mbugani jirani na bwawa la Irisya kijijini hapo, kundi la fisi lilishambulia na kuwaua ndama sita wa ng’ombe mali ya wanandoa hao.
Akielezea mkasa huo, Ramadhani Sinde, ambaye ni baba mzazi wa Hamida alisema kuwa baada ya mwanawe huyo kurejea nyumbani kutoka machungani alimweleza mumewe kuwa fisi walivamia kundi la ng’ombe alilokuwa akilichunga mbugani na kuua ndama sita.
“Kutokana na maelezo hayo, mumewe alimjia juu mkewe kwa kumtishia maisha... hakuridhika na utetezi wowote kwa vile aliamini huo ulikuwa ni uzembe tu wa mkewe kushindwa kuwazuia fisi hao,” alisema mzee Sinde na kuongeza;
“Alikasirika sana kiasi kwamba hakutaka hata mkewe alale naye chumba kimoja hivyo mama huyo akiwa na mwanawe mdogo wa mwaka mmoja alilazimika kulala sebuleni siku hiyo”.
Sinde alisema siku iliyofuata, Limu alimfukuza mkewe na kumtaka arejee kwao lakini baadaye alimfuata huko kwao na alipofika aliwaambia wazazi kuwa hamtaki tena Hamida kwa kuwa ni mfujaji wa mali zake hivyo apewe mke mwingine kutoka nyumba hiyo ili asirudishiwe mahari.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Irisya, Athuman Nkungu amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba Serikali ya Kijiji inafanya juhudi za kuwakutanisha wahusika wa pande zote mbili ili kutafuta suluhu ya suala hilo.
No comments:
Post a Comment