Taasisi ya Connected Farmer Alliance (CFA) ya ubia kati ya watu binafsi na makampuni inayohusisha Vodafone,Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) na shirika lisilo la kibiashara la TechnoServe yamesainiana makubaliano ya kwanza ya kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu kuongeza uzalishaji kwa maelfu ya wakulima wadogo wa vipato vya chini nchini Tanzania.
Kwa mujibu wa makubaliano kati ya CFA, Olam International
inayojishughulisha na masuala ya elimu kwa wakulima na ununuzi wa mazao na Vodacom Tanzania,wakulima wadogo 30,000 nchini Tanzania wa kahawa,pamba na Kakao wanaohudumiwa na kampuni ya Olam watanufaika na huduma mbalimbali kama vile,ushauri wa kilimo kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi na aarifa kuhusu ratiba za mafunzo na matukio yajayo.
Vingine ni taarifa kwa muda mwaafaka kuhusu mabadiliko ya bei ya mazao sokoni pia kuanzishwa kwa huduma ya kutuma na kupokea fedha kwa kutumia huduma ya Mpesa ya Vodafone badala ya fedha taslimu kuanzia Desemba 2014 na kuendelea,hivyo kuwawezesha wakulima kutunza pesa zao vizuri kwa usalama zaidi.
Chini ya ushirikiano huu TechnoServe itatoa mafunzo kwa wafanyakazi wa Olam International na wakulima nchini.