Ooh…nooo! Wachumba wa muda mrefu, staa wa sinema za Kibongo, Rose Donatus Ndauka na Malick Bandawe ambao maisha yao ya kimapenzi yamekuwa yakitawaliwa na msuguano wa chini kwa chini, hatimaye wameachana, Ijumaa leokwetu linakupa mkanda mzima.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini na cha uhakika kimemwaga data kwamba wachumba hao ambao walivalishana pete kwa mbwembwe miaka mitatu iliyopita huku wakipika na kupakua lakini wamekuwa katika mzozo wa muda mrefu wa kifamilia, ambapo mara kadhaa wameripotiwa kuchapana wameachana.
“Unajua hawa jamaa wamekuwa na maisha ya kutoaminiana sana, nadhani wivu ndiyo sababu kubwa, lakini naona safari hii hali imekuwa mbaya zaidi kwa sababu Rose ameamua kubeba kilicho chake na kuondoka kwa mwenzake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Hiyo ndiyo habari ya mjini, bidada karudi kwao (Kigogo, Dar) na mwanaye. Ilikuwa ni lazima ndoa isiwepo kwani licha ya kupata mtoto hakukuwa na furaha hata kidogo.”
TATIZO NI NINI?
Ingawa chanzo hicho hakikuweza kuingia kwa undani kuhusu tatizo hasa lililotokea safari hii, lakini kilibainisha kwamba kabla ya tukio la sasa, mzozo mwingine mkubwa uliibuka kati yao.
“Kuna kipindi hali ilikuwa tete sana, Malick akaamua kuchukua mabegi yake na kutokomea kusikojulikana ambako alikaa kwa muda wa kama wiki mbili.
“Haikujulikana alikuwa wapi kwa muda wote huo, lakini baadaye tukamuona jamaa anarudi na maisha yao yakaendelea.
NDOTO YA NDOA YAYEYUKA
“Lakini wakati bado mambo hayajatulia, kumeibuka tatizo lingine kubwa ambalo limesababisha Rose kuamua kuondoka huku ndoto ya ndoa ikiyeyuka,” kilisema chanzo hicho.
VIPI KUHUSU MTOTO?
Katika mtafaruku huo, Malick alikataa katakata mtoto wake kuondoka na mama yake, lakini kutokana na umri wa mwaka mmoja wa kijana wao huyo, Naveen, alilazimika kuondoka na mama yake kwa vile bado ananyonya.
Rose, mmoja kati ya waigizaji warembo wa filamu Bongo, inasemekana kwamba yupo nyumbani kwa wazazi wake, Kigogo kutoka kwa mchumba wake, anayeishi Tandale, Tanesco jijini Dar.
Baada ya kunyetishiwa ‘ubuyu’ huo, Ijumaa Wikienda lilizama mzigoni ambapo stepu ya kwanza ilikuwa ni nyumbani walikokuwa wakiishi wapenzi ambapo hawakuwepo.
JIRANI ANASEMAJE?
Akizungumza na gazeti hili juu ya kuondoka kwa Rose nyumbani hapo, mmoja wa majirani zake aliyejitambulisha kwa jina moja la Sudi alikuwa na haya ya kusema:
“Rose Ndauka ana muda hatumuoni kama miezi sasa lakini ‘mista’ tunamuonaona labda kama amehama ‘but’ sina uhakika sana.”
ROSE VIPI?
Katika kutafuta ukweli alitafutwa Rose kila kona baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani lakini jitihada ziligonga mwamba hivyo zinaendelea.
Mchumba mtu, Malick alipoulizwa juu ya ukweli wa sakata hilo, alikiri kutokea na kwamba baada ya jitihada zake nyingi za kulinusuru penzi lao kushindikana, amekubali matokeo.
“Nimejitahidi sana kumwelewesha Rose ili apate kunielewa, ajue namna ya maisha yalivyo, lakini imekuwa ni kama kutwanga maji kwenye kinu. Nimekubali yaishe.
“Kinachonisikitisha sana ni kuona kuwa mwanangu anakwenda kulelewa na mwanaume mwingine, inauma sana tena sana,” alisema bila kufafanua maana ya kauli hiyo.
Katika uchumba wao mrefu, Rose na Malick wamejaliwa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Naveen.