Kwa nini wanaume ni wagumu sana kufanya mambo ambayo wake zao wanawaomba au kuwataka kufanya? Jibu, ni kwa sababu ni wanaume na wameona baba zao wakifanya hivyo na wakaiga. Lakini jibu linaweza kuwa lingine, kutegemea na ufahamu wa mtu na hata mazingira. Lakini ukweli unabaki kwamba wanaume sio wepesi wa kutenda yale ambayo wanatakiwa na wake zao kutenda.
Siyo suala la kurithi, hapana. Ukweli ni kwamba, kutokana na mwanaume kutokuwa tayari kuongozwa au kumsikiliza mwanamke na kumkubalia, hatimaye imejijenga akilini na kuwa kama vile ni suala la maumbile. Ukweli ni kwamba, miaka mingi ya kutoamini kwamba, mwanamke anaweza, imefanya kuwe na kizuizi hicho kwenye akili ya mwanaume.
Utafiti wa hivi karibuni kwa mfano, ambao uliongozwa na Gavan Fitzsimons profesa wa masoko na saikolojia, kwenye chuo kikuu cha Duke, anasema, kinachotokea ni juhudi za mwanaume kutotaka kuingiliwa kwenye mambo yake, bila mwenyewe kujua kwamba, anafanya juhudi hiyo. Jambo hili kisaikolojia linafahamika kama reactance, ambapo mtu hufanya kinyume kabisa na anavyotakiwa kufanya. Ni juhudi za mtu kupinga kupewa amri au kuingiliwa katika uhuru wake.
Wataalamu wanasema kwamba, wanaume hujikuta tu wamepinga jambo la mke bila kujua hata sababu. Ndio maana wanaume wengi huharibikiwa kwa kukataa kufanya yaliyopendekezwa na wake zao na baadae hujiuliza ni kwa nini walikataa. Kwa hiyo wanaume wanapaswa sasa kujua kwamba, wanapombwa jambo na wake zao au kutakiwa kulifanya, wako kwenye hatari ya kulikataa. Kwa hali hiyo, wanapaswa kuwa waangalifu.
No comments:
Post a Comment