button

anim

Tally

advert2

security

Advert

Advert
Advert

babu

babu
leokwetu

mochrispoadver

pub

pub

flashplayer

Friday, November 7, 2014

AIBU:Ndege ya Rais wa China ilitumika kusafirishia meno ya Tembo

Ziara ya Rais Xi Jinping wa China aliyoifanya nchini Machi mwaka jana, imezua kizaazaa na kuitia ila sifa ya Tanzania kimataifa, baada ya maofisa waliokuwa wameambatana naye kuhusishwa na biashara haramu ya meno ya tembo.

Ripoti iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya Uingereza inayojihusisha na uchunguzi wa masuala ya mazingira, inadai kuwa maofisa hao walinunua kiasi kikubwa cha bidhaa hizo katika soko la Mwenge, Dar es Salaam, kisha kuzisafirisha kidiplomasia kwa ndege ya rais huyo.

Taasisi hiyo iitwayo Environmental Investigation Agency (Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira– EIA), katika ripoti hiyo inasema maofisa hao walitumia fursa ya kidiplomasia ya kutokukaguliwa kwa mizigo yao, kupitisha  bidhaa hizo haramu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).

Biashara ya meno ya tembo ilizuiwa kimataifa tangu mwaka 1989 kwa kusainiwa kwa azimio la kulinda viumbe walio hatarini (Cites), azimio ambalo pia limesainiwa na China na Tanzania.

Taarifa hiyo iliandikwa kwa mara ya kwanza jana na Gazeti la New York Times la Marekani na baadaye kuwa moja ya habari zilizopewa uzito wa juu katika vyombo vingine vya habari vya kimataifa, huku Kituo cha Televisheni cha Shirika la Habari la Uingereza BBC, kikijadili kwa kina kashfa hiyo iliyopewa jina la “ndege ya rais kutumika kusafirisha meno ya tembo”.

BBC katika taarifa yake ilitumia picha za meno ya tembo na zile za maktaba ambazo zilikuwa zikimwonyesha Rais Jinping akilakiwa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na viongozi wengine wa Tanzania alipowasili nchini kwa ziara hiyo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana kwamba Serikali haifahamu chochote kuhusu tuhuma hizo na kwamba hata kama zingekuwa na ukweli ndani yake waliopaswa kuulizwa ni Serikali ya China.

“Serikali haina evidence (ushahidi) wowote unaoonyesha kwamba suala la aina hii lilitokea, lakini pili mimi siamini kama kweli maofisa wa China walifanya kitendo hiki na kama hicho kilifanyika basi wanaopaswa kuulizwa ni Serikali ya China,” alisema Balozi Sefue na kuongeza:

“Siamini kama madai hayo ni ya kweli kwa sababu maofisa wanaosafiri na viongozi hukaguliwa, kwa nini wasikaguliwe na China ni marafiki zetu wazuri tu? Kwa hiyo sisi kama Serikali hilo jambo hatulifahamu kabisa.”

Baada ya kutangazwa katika vyombo vya habari vya kimataifa, maofisa wa Serikali ya China wamekanusha tuhuma hizo wakisema, “hazina ukweli wowote” wala ushahidi wa kuzithibitisha.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Hong Lei alinukuliwa na Shirika la Habari la Associated Press (AP) akisema: “Ripoti hiyo haina ushahidi wowote na hatukufurahishwa kabisa na taarifa hizi.”

Mkurugenzi wa usafirishaji wa viumbe walio kwenye hatari ya kutoweka nchini China, Meng Xianlin alipuuza madai hayo akisema: “Tuhuma pasipo ushahidi haziwezi kuaminika.”

Ununuzi wa nyara

Ripoti hiyo inayoitwa “Wanatoweka: Uhalifu, Rushwa na Kuangamizwa kwa Tembo wa Tanzania,” inadai kuwa ujumbe wa maofisa wa Rais Jinping ulifika nchini wiki mbili kabla ya ujio wa Rais huyo na kununua pembe za ndovu katika eneo la Mwenge ambalo ni maarufu kwa uuzaji vinyago.

Inadai kuwa ujumbe huo ulinunua meno ya tembo kwa Dola za Marekani 700 (sawa na Sh1,120,000) kwa kilo moja, bei ambayo ni mara mbili ya ile ya kawaida na kwamba Wachina hao walinunua maelfu ya kilo za meno hayo na kuyasafirisha kwa ndege ya Rais Jinping.

Mfanyabiashara katika eneo hilo, aliyetambulika kwa jina moja la Suleiman amenukuliwa katika ripoti hiyo akisema bei ya meno ya tembo ilipanda kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake wakati wa ziara hiyo.

Mtu mwingine ambaye hakutajwa jina lake katika ripoti hiyo anaeleza kuwa jambo hilo lilifanyika pia hata wakati wa ziara ya aliyekuwa Rais wa China, Hu Jintao mwaka 2009 ambako maofisa waliokuwa katika msafara huo walinunua bidhaa hizo.

“Wanakuja kuchukua vitu vingi, si kwa ajili ya Hu Jintao, bali kwa ajili yao. Baada ya hapo wanakwenda uwanja wa ndege na kupita bila kukaguliwa kwa sababu VIP hawakaguliwi,” alidai.

EIA katika taarifa hiyo pia inadaiwa kuwa Wanadiplomasia wa China pamoja na maofisa usalama wa nchi hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Tanzania walifanikisha upatikanaji na usafirishaji wa meno ya tembo kwenda China.

“Tanzania ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa kutoa meno ya tembo kwa wingi. Pia China ndiyo mnunuaji mkubwa wa meno ya tembo duniani,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo yenye kurasa 36.

No comments: